Na Sultani Kipingo, Globu ya Jamii

Mfanya biashara bilionea wa Nigeria Aliko Dangote amesema jambo la kwanza atalofanya endapo atafanikiwa kuinunua klabu ya Arsenal ya Uingereza ni kumtumbua kocha Arsene Wenger. 

 Toka mwezi Mei mwaka 2015 Dangote amekuwa akikaririwa mara kwa mara kuwa ana mipango ya kuinunua klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza ambayo mshika dau mkuu wake ni bilionea wa Kimarekani Stan Kroenke anayeshikilia hisa asilimia 67 za klabu hiyo. 

 January 18 mwaka huu alipoulizwa, bilionea huyo namba moja wa Afrika alinukuliwa na shirika la habari la CNBC akisema kwamba kwa sasa jicho lake kwanza liko kwenye kuifanya kampuni yake ya Dangote Group kuwa na kiasi cha dola bilioni 100 kabla ya kuinunua Arsenal. 

"Nitainunua (Arsenal) lakini kwanza nataka kuimarisha miradi yangu ambayo kwa sasa ni yenye thamani ya dola bilioni 18, ndipo nitaigeukia Arsenal” CNBC ilimkarriri Dangote wakati wa mkutano wa uchumi wa dunia huko Davos, Uswisi. 

 Dangote, ambaye ni shabiki wa Arsenal na sio tena wa kocha Wenger, ameteka tena vichwa vya habari karibuni kwa kusema jambo la kwanza atalofanya ni kubadili kocha. “Amefanya kazi nzuri, lakini mtu mwingine inabidi aje kujaribu bahati yake”, alisema alipohojiwa na Bloomberg. 

 Dangote amekuwa mkosoaji mkubwa wa Wenger, akimshauri kocha huyo Mfaransa ‘kubadili mfumo wake kidogo’ mnamo mwaka 2015. Lakini pamoja na kuonesha nia ya kuinunua Arsenal, bado hajaweka dau mezani. 

Yeye anasema atafanya hivyo mara tu ujenzi wa mradi wake mkubwa wa mitambo ya kuchakata mafuta wenye thamani ya dola bilioni 11 jijini Lagos utapokamilika. Kampuni yake ya Dangote Group ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa kampuni ndogo ya biashara, lakini leo imekuwa kubwa na yenye matawi nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Tanzania, Benin, Ghana, Nigeria na Togo. 

Hivi sasa pamoja na kuzalisha saruji kampuni hiyo inazalisha pia sukari na vyakula. Bilionea wa Kirusi Alisher Usmanov mwenye hisa asilimia 30 katika Arsenal aliweka dau la dola 2.6 billioni ili kuinunua Arsenal mapema mwaka 2017 lakini bilionea Kroenke mwenye hisa zaidi ya 67 aligoma.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...